"Tazama ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka..."
huwa nakaa nakumbuka wimbo huu nilipokuwa mdogo!!!!!
----------------------------------------
"Bongo sasa kumekucha bwana!" Hamidu aliyerejea hivi karibuni toka Tanzania kuona ndugu baada ya miaka 10 anamsimulia mtanzania mwenzake Joseph ambaye hajarudi nyumbani tangu alipoondoka miaka 7 iliyopita.
"aah! nasikia umeme wa mgao, maji ya shida, rushwa kama kazi, huduma mbovu za jamii!" Joseph anamjibu Hamidu. "Ajira shida kwa wasomi wanaomaliza vyuo".

Basi wanazungumza kwa muda mrefu sana, Hamidu anajaribu kumweleza Joseph mambo mengi mazuri yanayoendelea nyumbani na Joseph anamjibu kwa maneno yasiyo mazuri anayosikia na anayoyasoma kwenye vyombo tofauti vya habari. Hamidu anamalizia kwa kumwambia Joseph ana miaka miwili mpaka mitatu atarejea nyumbani kabisa. Joseph anasema akipata makaratasi atakuwa anakwenda kutembea na kurudi, lakini hapa ndio kafika!.
Katika kuishi kwangu nchi mbalimbali, nimekutana na akina Hamidu na Joseph wengi tu. Wote wawili wako sahihi kabisa na mambo wanayoyazungumzia, naamini kabisa kila mmoja wetu popote tulipo, kama tuko Marekani, Australia, Uingereza, Japan, au popote duniani tuna kahamidu au kajoseph ndani mwetu, wengine kadogo sana, wengine kawastani na wengine kakubwa sana.
Watanzania wengi tuko nje ya nchi yetu kwa kutafuta maisha mazuri ya sisi wenyewe na familia zetu. Tumekuja nje kwa kutumia njia na sababu tofauti, na kubaki au kurudi kunafuata sababu nyingi tofauti vilevile. Mimi nadhani popote mtu atakapoamua kuishi yeye na familia yake ni nyumbani. Nimekutana na watanzania wengi tu ambao wamekuwa raia wa nchi wanazoishi lakini mizizi yao wanajua iko Tanzania na wanaelewa kwamba wao ni watanzania kabla ya yote. Wanajiendeleza wao na ndugu na jamaa zao Tanzania.
Mimi nimeanzisha hii tovuti kwasababu kubwa zifuatazo, ambazo zilinisumbua na zingine bado zinanisumbua mimi binafsi kwa muda mrefu na nadhani kuna watanzania wengine wenzangu walio na matatizo kama yangu au na mengine tofauti ningependa kubadilishana nao mawazo na utatuzi;
-
Nilisumbuka kuanzisha kampuni Tanzania, kupata washirika na wafanyakazi waaminifu.
-
Ujenzi wa nyumba; kuanzia kiwanja, ramani, usimamizi wa ujenzi, upangishaji wa nyumba ilipokwisha.
-
Kupata bidhaa mbalimbali ninazohitaji huku kutoka nyumbani, mara nyingi inanibidi nisubiri mtu anayekuja la sivyo nilipie UPS au EMS.
-
Kupata kampuni zilizopo Tanzania ninazotaka kushirikiana nazo kufanyanazo biashara.
-
Kuagiza vitu ninavyohitaji Tanzania kutoka nchi za nje; Japan, Dubai au kutoka nchi zingine.
-
Nina ndugu yangu yeye tatizo lake kubwa lilikuwa kutafuta ajira nyumbani wakati bado yuko nje akimalizia elimu yake.
Wahenga walisema, "Penye nia pana njia". Nilichofanya ili niweze kutatua matatizo yangu ni kufanya utafiti wa makini sana, mimi na wenzangu tumefanikiwa kuanzisha kampuni inayoitwa SisiMizi TZ. Tumeweza kupata washirika na washauri wa uhakika katika shughuli na nyanja mbalimbali zinazotuhusu sisi binafsi na jamii yetu kwa ujumla kwa faida yetu sote.
Nimewaomba washirika na washauri hao wachangie katika gazeti-pepe la kila mwezi nitakalokuwa natuma bure kwa mtu yeyote atakayehitaji. Naamini wakati muafaka umefika watanzania kuanza kushirikiana kwa mawazo, masoko na kwa vitendo. Katika kusafiri kwangu na kukutana na watanzania, wengi wetu tunataka au tunafanya kitu fulani iwe ni pale tunapoishi au nyumbani. Kitu nilichogundua ni maendelea tunayopata ni kidogo au ya wastani kwa sababu kila mmoja wetu anajaribu kufanya kila kitu peke yake!
Nia kubwa ya hii tovuti ni kutuunganisha watanzania tunaotaka maendeleo na kuamini kwa dhati kwamba tukishirikiana kwa bidii na uaminifu tutafanikiwa wote zaidi.
Wahenga walisema, "Umoja ni nguvu utengano ni dhaifu"